Real Madrid Yatinga Fainali Ligi ya Mabingwa, Yaiduwaza Man City

471

Waswahili husema sikio la kufa halisikii dawa, pengine ni kauli ambayo unaweza kuitumia kuelezea mikasa ya kujirudia ya kutolewa kwa kikosi cha Manchester City kwenye hatua muhimu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya Leo Jumatano kukubali kufungwa bao 3-1 na Real Madrid.

Manchester City inayonolewa na kocha Pep Guardiola iliingia dimba la Santiago Bernabeu ikiwa na faida ya goli moja baada ya mchezo wa awali uliopigwa Etihad City kushinda goli 4-3 lakini mtanange wa marudiano wakaweza kupata bao la kuongoza tena kabla ya mambo kuharibika kwa kuruhusu goli za jioni kabisa.

Alianza Riyard Mahrez kufunga goli akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno Benardo Silva kisha winga ingizo jipya Rodrygo kukwamisha mpira wavuni kwa pasi ya Karim Benzema kisha Rodrygo akarudi tena kambani kwa krosi maridadi ya beki Carvajal.

Baada ya bao hilo, mchezo ukalazimika kwenda muda wa ziada ambapo makosa ya Ruben Dias kwenye kipindi cha kwanza muda wa ziada yaliwapa faida Madrid kwa kupata tuta ambalo lilikwamishwa kwa ustadi mkubwa na Benzema ambaye linakuwa bao la 43 katika mashindano yote msimu huu.

Kwa maana hiyo, Real Madrid wamefuzu fainali kwa jumla ya goli 6-5 na watacheza na Liverpool fainali ya Uefa ambayo itapigwa Ufaransa Mei 25, fainali ambayo itakuwa na kumbukumbu ya mwaka 2018 ambapo Madrid walishinda kwa bao 3-1.

Author: Bruce Amani