Real waichapa Osasuna 2-0, safarini kuwafuata Chelsea Ligi ya Mabingwa

Real Madrid imeendelea kuwapa presha ya ubingwa vinara Atletico Madrid baada ya kushinda goli 2-0 dhidi ya Osasuna mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania La Liga.

Goli la mlinzi Eder Militao akimalizia kwa kichwa kona ya kiungo Isco na kiungo mkabaji raia wa Brazil Casemiro akimalizia pasi ya Karim Benzema yalitosha kutoa alama tatu mbele ya Osasuna ambao kwa dakika nyingi walikuwa imara.

Atletico walipata ushindi wa kukwea mpaka nafasi ya kwanza kwa tofauti ya alama tano mapema Jumamosi kwa kuifunga Elche 1-0.

Barcelona, walipoteza nafasi ya kwenda kileleni Jumanne kwa kukubali kipigo cha goli 2-1 wakiwa nyumbani Camp Nou, na wanaweza kutoshana na Madrid kwa alama endapo watashinda mechi yao ya Jumapili Valencia.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane na kikosi chake watasafiri kuwafuata Chelsea London katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mkondo wa pili baada ya raundi ya kwanza kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

 

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares