Real yaifyeka Atletico na kuibuka kidedea derby ya Madrid

Bao la 100 lake Gareth Bale katika klabu ya Real Madrid liliisaidia kuvuna pointi zote tatu katika mtanange mkali wa watani wa Madrid dhidi ya Atletico na kuwapiku mahasimu wao hao hadi nafasi ya pili. Casemiro aliwaweka Los Blancos kifua mbele kwa kufunga bao safi la tikitaka lakini Antoine Griezmann akawasawazishia Atletico baada ya kubaki yeye na kipa Thibaut Courtous.

Sergio Ramos aliwarejesha wageni kifua mbele kwa kusukuma wavuni mkwaju wa penalty huku Bale akimalizia kazi nyuzi kutokana na pasi ya Luka Modric.

Atletico walimaliza mchezo na wachezaji 10 baada ya Thomas Partey kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano. Real sasa wameshinda sita kati mechi zao saba za mwisho, na hata kutoka sare ya 1 – 1 na Barcelona katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Copa del Rey. Ushindi huu wa derby ya Madrid unawaweka nyuma ya vinara wa La Liga Barcelona na pengo la pointi tano.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends