Rodrygo Aiadhibu Chelsea, Real Yatinga Nusu Fainali

77

Chelsea imeondolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchapwa bao 2-0 na mabingwa watetezi Real Madrid katika mchezo wa mkondo wa pili a robo fainali uliochezwa uwanja wa Stamford Bridge Leo Jumanne.

Chelsea ambayo kwa sasa inanolewa na kocha wa muda Frank Lampard kabla ya mchezo huo walikuwa wamefungwa bao 2-0 walizozipokea dimba la Santiago Bernabeu ambapo walikuwa kwenye uhitaji wa ushindi ili kutinga hatua inayofuata.

Mabao mawili ya kipindi cha pili yaliyofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Rodrygo yametosha kudidimiza jahazi la Lampard nyumbani mbele ya mmiliki wa klabu hiyo bilionea Todd Boehly.

Rodrygo alifunga bao la kwanza akitumia pasi ya Vinicius Jr baada ya mchezo wa kushtukiza kabla ya kutupia tena akitumia pasi isiyo na choyo kutoka kwa kiraka Federico Valverde dakika 10 kabla ya mpira kumalizika.

Kwa matokeo hayo, Real Madrid itacheza na mshindi kati ya Manchester City ama Bayern Munich katika hatua ya nusu fainali ya msimu huu 2022/23.

Author: Bruce Amani