Ronaldo aandika rekodi, Juventus ikipigwa 2-1 na Napoli

Mbio za ubingwa wa Seria A ziko kwenye rehani baada ya matokeo ya timu zote mbili zilizo kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa kuyumba, Juventus imepigwa wakati Inter Milan imetoa sare.

Juventus ambayo takribani miaka nane wametawala soka la Italia wameshindwa kuongeza tofauti ya pointi na Inter Milan ambayo ilitoa sare mchezo wa mapema wikendi hii dhidi ya Cagliari ambapo nao (Juventus) wamekutana na kichapo kutoka kwa Napoli cha goli 2-1.

Matokeo ya kupoteza kwa Juve yanatoa mwanya wa tofauti ya alama tatu pekee ambapo ingeshinda jana Jumapili ingetokea tofauti ya alama sita wakifuatiwa na Inter Milan.

Piotr Zielinski aliipa Napoli goli la uongozi kabla ya Lorenzo Insigne kufunga goli la pili na la ushindi pia. Wakati muda ukiyoyoma Cristiano Ronaldo alifunga goli la nane mfululizo ndani ya Seria A na goli la kufutia machozi kwa Kibibi kizee cha Turin.

Goli la Ronaldo linamfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Juventus kufunga goli nane mfululizo Seria A  tangu alipofanya hivyo David Trezeguet mwaka 2005.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends