Ronaldo aipa ushindi Ureno jioni, agusa anga la Sergio Ramos

26

Cristiano Ronaldo amevunja rekodi ya ufungaji katika michezo ya timu za taifa kwa upande wa wanaume baada ya kufunga goli mbili katika ushindi muhimu wa bao 2-1 walioupata Ureno dhidi ya Jamhuri ya Ireland kuwania kufuzu Kombe la Dunia mtanange uliopigwa Jumatano Septemba Mosi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36, alifunga goli zote mbili kwa kichwa na kufikisha bao 28 kwa kichwa ngazi ya taifa, akivunja na kuweka rekodi yake kwa bao 110 na 111.

Awali rekodi ya kufunga goli nyingi ilikuwa inashikiliwa na Ali Daei, ambaye alifunga bao 109 akiwa Iran katikati ya mwaka 1993-2006, itakumbukwa rekodi hiyo ya mabao ilifikiwa na Ronaldo baada ya kufunga bao mbili kwenye mechi dhidi ya Ufaransa kwenye Euro 2020.

Ronaldo ambaye mwanzoni mwa wiki hii amekamilisha kujiunga na Manchester United pia amefikia rekodi ya beki wa Real Madrid Sergio Ramos ya kucheza mechi nyingi, ambapo Mreno huyo amecheza mechi 180.

Author: Asifiwe Mbembela