Ronaldo avunja rekodi ya Trezeguet Juventus

Cristiano Ronaldo amefunga goli mbili kwa penati na kuongeza urefu wa rekodi yake ya kufunga goli 10 mfululizo kwenye mechi 6 akiisaidia Juventus kushinda goli 3-0 dhidi ya Fiorentina.

Wenyeji walianza kupata goli la kwanza baada ya mpira kumgonga mkononi mlinzi wa Fiorentina, Ronaldo akakwamisha mpira huo nyavuni.

Rodrigo Bentancur aliangushwa kwa kumi na nane kuelekea tamati ya mchezo huo, Ronaldo akafunga goli la pili.

Goli la tatu likawekwa kimiani na ingizo jipya la Matthijs de Ligt kwa kichwa kufuatia mpira wa kona.

Ronaldo amefikia rekodi ya kufunga goli 9 mfululizo za Seria A za Juventus, anakuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo tangu mwaka 2005 alipofanya hivyo David Trezeguet.

Magoli ya leo yanamfanya Cristiano Ronaldo kufikisha goli 50 kwenye mechi 70 tangu alipojiunga na Juventus mwaka 2018.

Ndani ya msimu huu kwa ujumla Ronaldo amefunga goli 33 katika mechi 33 katika ngazi ya taifa na klabu.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends