Ronaldo, Benzema waipamba mechi ya Ufaransa, Ureno

452

Jina la Cristiano Ronaldo limekuwa likitajwa sio Leo bali siku nyingi na sasa limeendelea kutajwa baada ya kuhusika moja kwa moja kuinusuru Ureno kutoka kwenye dimbwi la kipigo kutoka kwa Ufaransa katika mechi ya mwisho ya kundi F mashindano ya Euro 2020.

Kutajwa kwa Ronaldo kunatokea baada ya kufunga goli mbili katika sare ya bao 2-2 dhidi ya Ufaransa mchezo uliopigwa Leo Jumanne huku Ufaransa wakipata bao kupitia kwa Karim Benzema kwa penati na kufunga akimalizia pasi ya Paul Pogba.

Ronaldo anafikisha goli 108 ambapo limebakia bao moja kufikia rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Iran Ali Daei aliyeweka rekodi hiyo kuanzia mwaka 1993-2006.

Katika mchezo uliokuwa wa aina yake huku timu zikabadilishana nafasi ya kukaa kileleni kutokana na matokeo ya wakati huo, ilikuwa filimbi ya mwisho ya mwamuzi kutamatisha kandanda kuashiria matokeo kuwa 2-2.

Matokeo hayo yanaifanya Ufaransa kumaliza nafasi ya kwanza, Ujerumani nafasi ya pili kwa alama nne lakini wanafanana na Ureno tofauti iliyopo ni rekodi ya ana kwa ana(head-to- head).

Author: Asifiwe Mbembela