Rummenigge: Flick kuendelea kuinoa Bayern kwa sasa

Bayern Munich walipata ushindi rahisi wa mabao manne kwa sifuri dhidi ya watani wao Borussia Dortmund. Baada ya mechi hiyo maarufu kama Der Klassiker, mwenyekiti wa klabu hiyo Karl Heinz Rummenigge alisema kaimu kocha Hansi Flick ataendelea kukinoa kikosi hicho kwa sasa. Klabu hiyo iliwachana na kocha wake Niko Kovac hivi karibuni.

Flick alipata ushindi huo mnono katika mechi yake ya kwanza ya Bundesliga baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Olympiakos katika hatua ya makundi ya Champions League na wakafuzu katika hatua ya mchujo.

Robert Lewandoswki aliiangamiza timu yake ya zamani kwa kufunga mabao mawili, Serge Gnabry akafunga jingine huku beki wa BVB Mats Hummels akijifunga katika lango lake mwenyewe

Katika matokeo mengine ya Bundesliga jana, Hertha BSC ilifungwa mabao 4 kwa 2 na RB Leipzig 2, Mainz ikalazwa mabao matatu kwa mawili na Union Berlin, Schalke ikalazimisha sare ya 3 – 3 na Düsseldorf na Paderborn ikapoteza bao moja kwa sifuri dhidi ya Augsburg. Katika mechi ya leo, Borussia Moenchengladbach itashuka dimbani dhidi ya Werder Bremen, Wolfsburg itaialika Bayer Leverkusen na Freiburg itaikaribisha Eintracht Frankfurt.

Author: Bruce Amani