Rwanda yaingia mkataba na PSG kutangaza utalii

Rwanda leo imesaini mkataba na timu ya Ufaransa ya Paris St. Germain, PSG kwa lengo la kuutangaza utalii wa taifa hilo la Afrika Mashariki. Mkataba wa aina hiyo ni wa pili kusainiwa na Rwanda kwa mwaka huu. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Clare Akamanzi amesema wanawekeza sehemu ya mapato ya utalii wao katika ushirikiano wa kimkakati kama mkataba walioingia na klabu hiyo ya Ufaransa kwa sababu wanaelewa matokeo mazuri katika mtazamo jumla wa nchi hiyo ulimwenguni.

Akamanzi hakusema ni pesa kiasi gani Rwanda itatoa katika mkataba huo. Aidha, duru za karibu na klabu hiyo zimesema mkataba huo ni kati ya Euro milioni 8 na Euro milioni 10. Chini ya mkataba huyo klabu ya PSG itatangaza bidhaa za Rwanda, huku ujumbe unaoitangaza Rwanda utawekwa kwenye jezi za timu yake ya wanawake na kwenye uwanja wa PSG.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends