Safari ya matumaini kwa Madagascar yaishia njiani

53
Tunisia imetinga nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika – Afcon 2019 baada ya kuifunga timu iliyokuwa ya kushangaza kwenye michuano hii Madagascar kwa goli 3-0 katika mchezo uliofanyika dimba la Al Salaam.
Ushindi wa Tunisia unaifanya timu hiyo kufuzu nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 2004, miaka 15 sasa ikiwa imepita bila kufanya hivyo huku mwaka huo ikitawazwa kuwa Mabingwa wa taji hilo
Baada ya Madagascar kushindwa kucheza mpira wao uliozoeleka katika kipindi cha kwanza, Tunisia waliigundua njia kunako dakika za kipindi cha pili ambapo waliweza kufunga goli zote tatu kupitia kwa Ferjani Sassi, Strika Youssef Msakni na Naim Slitti.
Licha ya kupoteza nafasi ya kutwaa taji kwa kufungwa na Tunisia, bado Madagascar wanaondoka Misiri kama washindi baada ya kuishangaza dunia kwa namna ilivyokuwa ikipata matokeo huku ikiwa mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo katika historia ya timu hiyo.
Tunisia watakutana na Senegal siku ya Jumapili katika dimba la June 30 Cairo mtanange wa nusu fainali kabla ya ule mwingine Nigeria dhidi ya Algeria.

Author: Bruce Amani