Salah atupia mbili, Liverpool ikishinda 3-2 kwa Atletico

Kikosi cha Liverpool kimefanikiwa kuondoka na ushindi wa goli 3-2 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi uliopigwa dimba la Wanda Metropolitano huku vijana wa kocha Diego Simeone wakimaliza dakika 90 wakiwa pungufu.

Magoli mawili ya Majogoo wa Jiji la Merseyside Liverpool yakiwekwa kimiani na nyota wa kimataifa wa Misri Mohamed Salah ambaye sasa anakuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufunga goli angalau moja kwenye mechi tisa, bao lingine likiwekwa na kiungo mkabaji Naby Keita.

Ukiwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa na ubora mkubwa hasa eneo la ushambuliaji ambapo magoli mawili ya Atletico Madrid yakiwekwa kimiani na Antoine Griezmann.

Ushindi wa kikosi cha Liverpool unamfanya kocha Jurgen Klopp kufikisha mechi 21 bila kupoteza katika mashindano yote na wikiendi hii atakuwa ugenini kwenye dimba la Old Trafford kumenyana vikali na Manchester United Ligi Kuu England.

Silaha kubwa kwa Klopp ni ubora wa eneo la ushambuliaji ambapo kwenye mechi tisa za mwisho Liverpool imefunga mabao 30, ambapo wamefunga angalau goli tatu katika mechi saba za ugenini ikiwa ni rekodi ya aina yake.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends