Samatta atupia Ulaya, kinara wa magoli Ubelgiji

198

Mbwana Ally Samatta mshambuliaji wa Genk ya Ubeligiji kutoka Tanzania ameendelea kuwa mwiba mkali katika ligi ya Ubeligiji, Jupiler Pro baada ya kufunga goli 1 kati ya 4 ambayo klabu yake ya Genk ilishinda dhidi ya Royal Antwerp katika mchezo wa “Play Off”

Goli alilofunga jana linamfanya kufikisha goli 23 ambapo mchezaji anayemfuatia ana goli 18 pekee. Endapo ligi itamalizika hivi, Mbwana Samatta atakuwa mchezaji wa kwanza kutwaa kiatu cha dhahabu katika ligi kubwa ulaya akitokea Tanzania.

Mbali na Samatta katika mchezo huo straika wa Ukraine Rusland Malinovskiy alianza kufungua akaunti ya magoli kwa Genk kunako dakika ya 25 ya mchezo kwa penati huku mchezaji wa Ubeligiji Bryan Heynen akitumbukiza mpira kimiani katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili kwa penati tena.

Straika Junya Ito raia wa Japan alifanikiwa kufunga dakika mbili baada ya Samatta kufunga dakika ya 55 na Ito akaongeza dakika ya 57 ya mchezo na kufanya mpira kumalizika kwa jumla ya goli 4-0 dhidi ya Royal Antwerp.

Klabu ya Genk ilimaliza msimu wa kawaida kama vinara kwenye ligi yenye timu 16, wanaoenakana kuimarika zaidi katika hatua hii ya mtoano ambapo wakifanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu itakuwa mara ya nane.

Mpaka sasa timu hiyo inaongoza kundi ikiwa na alama 50, pointi tisa kamili kwa timu iliyo nafasi ya pili Club Brugge ambayo ina mechi mkononi, zimesalia mechi 3 kumalizika hatua ya mtoano. Timu yenye alama nyingi hutawazwa kuwa bingwa huku zenye alama ndogo hushuka daraja.

Author: Bruce Amani