Samatta, Mpole Watupia Stars Ikiichapa Afrika ya Kati 3-1

307

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) katika mchezo wa kirafiki mtanange uliopigwa Leo Jumatano katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Taifa Stars yamefungwa na kiungo Novatus Dismas Miroshi anayekipiga kunako klabu ya Beitar Tel Aviv Bat Yam FC ya Israel dakika ya 10 na washambuliaji, Nahodha Mbwana Ally Samatta wa Royal Antwerp ya Ubelgiji dakika ya 63 na George Mpole Mwaigomole wa Geita Gold ya nyumbani dakika ya 90.

Goli la George Mpole linakuwa la kwanza katika mechi ya kwanza akiitumikia timu ya taifa ya Taifa Stars kwa mara ya kwanza ambapo msimu huu amekuwa kwenye ubora mkubwa.

Bao pekee la Jamhuri ya Afrika ya Kati limefungwa na mshambuliaji wa Gasogi United ya Rwanda, Christian-Theodor Yawanendji-Malipangou kwa penalti dakika ya 66.

Stars iliyo chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen itacheza mechi mbili zaidi katika kalenda hii ya FIFA, nyingine dhidi ya Botawana Jumamosi na dhidi ya Sudan Machi 29, zote Uwanja wa Benjamin Mkapa pia.

Nazo Jamhuri ya Afrika Kati na Sudan zitamenyana Jumamosi.

Author: Asifiwe Mbembela