Sanchez: Nilitaka kuondoka Manchester United baada ya siku ya kwanza ya mazoezi

219

Mshambuliaji wa  Inter Milan ya Italia Alexis Sanchez amesema alikuwa tayari kuondoka Manchester United baada ya kipindi kimoja tu cha mazoezi na timu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza.

Sanchez,  mchezaji wa kimataifa wa Chile alijiunga na United Januari mwaka 2018 baada ya kufunga mabao 80 katika muda wa miaka mitatu na nusu (3-1/2) na klabu ya Arsenal ya mjini London, lakini alishindwa kung’ara chini ya makocha Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer, akimudu kuyafunga mabao matano tu katika michezo 45 na Manchester United.

Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona alijiunga na klabu ya Inter Milan kwa mkopo mwanzoni mwa msimu wa 2019 hadi 2020, kabla ya klabu hiyo ya Serie A nchini Italia kumsaini mwezi Agosti kwa mkataba wa kudumu wa miaka mitatu.

“Nilikubali fursa ya kwenda United, nilivutiwa na ilikuwa hatua nzuri kwangu.. lakini sikuuliza kuhusu kile kinachotokea ndani ya klabu,” Sanchez alinukuliwa na Sky Sports akiyasema hayo katika mtandao wake wa Instagram.

“Wakati mwingine kuna vitu ambavyo huwezi kuvitambua hadi ufike hapo, na nakumbuka mazoezi ya kwanza niliyokuwa nayo, niligundua vitu vingi. Alisema Sanchez kupitia Instagram.

“Baada ya mazoezi nilifika nyumbani na nikawaambia watu wa familia yangu na wakala wangu,  je mkataba wangu na Arsenal hamjauchana, ili nirudi huko? ” Walicheka, nikawaambia kuna kitu ambacho hakijakaa sawa.

“Lakini tayari nilisaini, nilikuwa tayari huko. Baada ya miezi michache ya kwanza niliendelea kuwa na hisia hizo hizo, hatukuwa na umoja kama timu wakati huo.”

Inter Milan iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi ya Serie A msimu uliopita, wataanza msimu mpya ugenini kwa Benevento iliyopanda daraja, mnamo Septemba 20.

Chanzo/Reuters

Author: Bruce Amani