Sancho atambulishwa rasmi Manchester United

Manchester United imemtangaza rasmi winga wao mpya Jadon Sancho kuwa mchezaji wao ikiwa ni takribani wiki mbili tangia usajili wa ada ya pauni milioni 73 kukamilika kutokea Borrussia Dortmund kutua viunga vya Old Trafford.

 

Baada ya kutambulishwa amesema kujiunga na Manchester United ni sawa na kutimiza ndoto zake. Amehamia Kaskazini Magharibi ya England baada ya kudumu kwa muda nchini Ujerumani.

 

Sancho anakuwa mchezaji wa pili kwa gharama kubwa ndani ya Manchester United na England nyuma ya mchezaji mwenza Harry Maguire. Amesaini mkataba wa miaka mitano kukiwa na kipengele cha kuongezwa mwaka mwingine mmoja.

 

“Nawashukuru sana Dortmund kwa kunipa nafasi ya kuonekana, ingawa nilijua kuna siku nitarejea England,” amesema Sancho mwenye umri wa miaka 21.

 

“Nafasi ya kujiunga na Manchester United nikutimiza ndoto zangu, nimejawa na shauku ya kuanza kuitumikia klabu hii”.

 

Usajili huo unatamatisha saga ya usajili wake ambapo msimu uliopita dakika za jioni, klabu ya Dortmund ilibadilisha maamuzi ya kumuuza kufuatia Manchester United kushindwa kufika dau hitajika.

 

Sancho alifunga bao 50 na asisti 57 katika mechi 137 ndani ya Borrusia Dortmund.

 

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema “Old Trafford itampa nafasi ya kuonyesha kile alichonacho (nafasi) ya kutosha”.

 

Unakuwa usajili wa kwanza kwa Manchester United msimu huu ingawa wamekuwa wakihusishwa na Raphael Varane wa Real Madrid pamoja na Harry Kane wa Tottenham Hotspur.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares