Semenya apoteza rufaa dhidi ya kanuni za homoni za kiume

Mwanariadha wa Afrika Kusini Caster Semenya amepoteza kesi yake ya rufaa ya kupinga kanuni zinazolenga kupunguza viwango vya homoni za kiume mwilini katika baadhi ya wanariadha wa kike.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro Michezoni limetoa uamuzi wa kina na kuyatupilia mbali maombi ya usuluhishi kutoka kwa Semenya na Shirikisho la Kimataifa la Riadha – IAAF.

Katika uamuzi wake, mahakama imesema kanuni zinazopendekezwa za IAAF kuhusu wanariadha wenye tofauti za ukuaji wa homoni za jinsia, ni za kibaguzi lakini zinapaswa kutumika.

Majaji wawili dhidi ya mmoja walitoa uamuzi kuwa kwa msingi wa ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, ubaguzi wa aina hiyo ni mbinu inayohitajika na yenye maana inayoweza kutimiza lengo la IAAF la kudumisha uadilifu wa wanariadha wa kike katika mashindano yanayozingatia kanuni zilizowekwa.

Sasa mshindi huyo wa Olympiki, dunia na mashindano ya jumuiya ya madola kwa mita 800 pamoja na wanariadha wengine wenye jinsia zaidi ya moja (DSD) – watalazimika kupata matibabu ili kkushiriki mashindano ya kuanzia mbio za mita 400 hadi maili, au wabadili mbio.

Author: Bruce Amani