Mane aiadhibu Uganda na kuipeleka Senegal robo fainali

Timu ya taifa ya Senegal imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika Afcon 2019 baada ya kuifunga Uganda The Cranes goli 1-0 katika mchezo wa 16 bora uliochezwa leo Ijumaa nchini Misri.

Senegal imepata ushindi huo kupitia goli la kipindi cha kwanza lililofungwa na staa wa Liverpool ya England, Sadio Mane kunako dakika ya 15 kabla ya kukosa penati katika kipindi cha pili kwa kupanguliwa na mlinda mlango Denis Onyango.

Simba wa Milima ya Teranga watajilaumu wenyewe kwa kutotumia nafasi vyema hasa kipindi cha kwanza baada ya kosa kosa za hapa na pale kupitia kwa Mane mwenyewe na Niang.

Aidha, Uganda imeondoshwa rasmi katika mashindano hayo kutokana na kipigo hicho licha ya kuonyesha kandanda safi kwenye michezo ya awali, inaungana na Mataifa ya Tanzania, na Kenya kufungwa na Senegal baada ya timu hizo mbili kupoteza mechi zake katika hatua ya makundi.

Kwa matokeo hayo sasa Senegal itacheza ya taifa la Benin katika hatua ya robo fainali baada ya Benin kuitoa taifa gumu la Morocco kwa mikwaju ya penati baada ya kumalizika kwa dakika 90 kwa sare ya goli 1-1.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments