Sergio Ramos akosa penati mbili Uhispania ikibanwa na Uswisi

Mlinzi kitasa Sergio Ramos alishuhudia matuta yake mawili yakiokolewa katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya dhidi ya Uswisi huku akiandikisha rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi ngazi ya taifa.

Mtanange huo ulimalizika kwa sare ya goli 1-1, ambapo Ramos alifikisha mechi ya 177 na kumfanya kuwa mchezaji mwenye mechi nyingi kimataifa na akimpiku kipa wa Juventus Gianluigi Buffon aliyekuwa anashikilia rekodi hiyo.

Kabla ya penati mbili kuokolewa, Ramos ambaye ni nahodha wa kikosi cha Real Madrid alikuwa amefunga penati 25.

Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 34, tuta la kwanza alijaribu kupiga pembeni lakini mlinda mlango Yann Sommer aliiona na kuokoa, wakati tuta la pili alitaka kupiga tuta kwa njia ya panenka.

Kocha wa Hispania amemtetea mlinzi wake akisema “takwimu zinambeba Ramos, nadhani ingetokea ya tatu angefunga bila shaka” Luis Enrique.

Author: Bruce Amani