Sevilla yachukua usukani La Liga

Sevilla imewaduwaza wengi baada ya kushika usukani wa ligi ya Uhispania, La Liga Jumapili baada ya kuwachabanga Celta Vigo kwa mabao 2-1, huku mabingwa watetezi, Barcelona wakitoka sare ya 1-1 dhidi ya Valencia, na wakiwa hawajashinda michezo minne iliyopita.

Atletico Madrid, iliungana na Barca kwa kuwa na pointi 15, baada ya ushindi mwembamba wa 1-0, wakiwa nyumbani dhidi ya Real Betis, kufuatia shuti la dakika za lala salama la Angel Correa, na kupanda hadi nafasi ya tatu, ikiipiku Real Madrid, kwenye kinyang”anyiro kikali cha ligi, ambapo timu sita za juu zinapishana kwa pointi mbili mbili.

Barca iliendelea kupoteza nafasi, lakini ilipata tena ujasiri kwenye mchezo huo baada ya shuti hatari katika dakika ya 23 lililopigwa na Messi, ambaye katika siku za karibuni amekuwa moto wa kutoea mbali na kadhihirisha hilo katika mtanange dhidi ya Tottenham Hotspurs siku ya Jumatano.

Hata hivyo walishindwa kuizuia Valencia, iliyokuwa imejipanga bara bara na kutoka nao sare, hivyo kikosi hicho kukijikuta kikimaliza ama na sare au kupoteza mechi kwenye michezo minne ya ligi, hii ikiwa ni muda mrefu zaidi bila ya ushindi tangu 2016.

Kocha wa Barca, Ernesto Valverde amesema “katika msimu huu inaonekana kuwa tunalazimika kutoka nyuma katika kila mchezo, na tunaogelea tukipishana na mawimbi, lakini tunajua kwamba hii itabadilika“.

Sevilla wanaongoza ligi wakiwa na pointi 16, wakati Barca wakiwa na pointi 15 sambamba na Atletico Madrid, lakini wanashika nafasi ya pili kutokana na tofauti ya wingi wa magoli. Real Madrid iliyochapwa 1-0 na Alaves juzi Jumamosi, inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 14, sawa na Alaves na Espanyol.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends