Sevilla yakamata nafasi ya kwanza La Liga

Sevilla imekamata usukani wa La Liga baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi za Real Valladolid Jumapili. Sasa wanaongoza na pengo la pointi moja dhidi ya nambari mbili Barcelona. Mreno Andre Silva aliwafungia Sevilla bao safi la kichwa na sasa wanaongoza msimamo wa ligi na pointi 26 baada ya mechi 13, Barca ambao walitoka sare ya 1-1 na Atletico Madrid ni wa pili na 25.

Atletico Madrid wanashikilia nafasi ya tatu na pointi 24 huku mabingwa wa Ulaya wanaoyumba Real Madrid wakiridhika na nafasi ya sita na pointi 20 baada ya kichapo cha 3-0 na Eibar.

Kwingineko, Espanyol ilikosa nafasi ya kurejea katika nafasi nne za kwanza baada ya kuzabwa 3-1 na Girona. Cristhian Stuani alifunga mabao mawili na kumpiku Messi kama mfungaji wa mabao mengi kwenye La Liga, akiwa na 10.

Villareal ilipata ushindi muhimu wa 2-1 dhidi ya Real Betis ushindi ambao umewaweka pointi tatu juu ya eneo la kushushwa ngazi katika nafasi ya 16.

Athletic Bilbao, bado wanasaka ushindi wa kwanza tangu mwanzo wa msimu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Getafe, maana kuwa vijana hao ambao hawajawahi kushushwa ngazi, wangali katika eneo hatari na pointi 11.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends