Shangazi ajaza pengo la Barbara kwenye bodi ya Simba

Hatimaye Rashid Abdallah Shangazi ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba akichukua nafasi ya Barbara Gonzalez Leo Alhamis Julai 22, 2021.

Shangazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mlalo, na Mwenyekiti wa tawi la Simba Bungeni maarufu ‘Wekundu wa Mjengoni’ ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na taarifa yake kuwekwa kwenye mitandao rasmi ya klabu.
Kupitia ukurasa wao wa mitandao ya kijamii wa Simba wameandika Shangazi ni mtu anayeamini katika kufanya kazi kwa umoja na kuongoza umma kwa nguvu ili kuleta mafanikio chanya na haogopi kuchukua hatua yoyote.
Wameongeza kuwa pia ana uwezo wa kufanya kazi kwa kujitegemea katika mazingira ya mabadiliko na changamoto kwenye muda uliowekwa na vipaumbele.
Kuhusu uzoefu wake Simba wamesema ana ujuzi mzuri wa masuala ya Uendeshaji wa Biashara na mwenye shauku ya kusaidia makundi mbalimbali katika jamii ili kufikia malengo yao. “Yeye ni mtu bora anayetamani kutoa ubora katika kila fursa,” wameeleza Simba
Barbara aliteuliwa kushika nafasi hiyo Septemba 5, 2020 na kuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi hiyo kubwa kwa ngazi za klabu za Ligi Kuu.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares