Sharks wazamishwa Bandarini katika KPL

117

Klabu ya Bandari imeizamisha Kariobangi Sharks 1-0 uwanjani Kasarani na kupaa kileleni mwa ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu.

Yemi Mwana alipachika bao la kipekee dakika ya 71 vijana wa Bernard Mwalala wakilipiza kisasi dhidi ya Sharks ambao waliwapiku kwa goli hilo moja na kuwai kombe la SportPesa mwezi jana jijini Dar es Salaam.

Bandari sasa wana pointi 28, alama tatu mbele ya Mathare United baada ya mechi 13. Mathare wanasafiri mjini Kericho kuchuana na Zoo FC.

Sofapaka, ambao wanamenyana na bingwa Gor Mahia hapo kesho Jumapili ugani Afraha katika kaunti ya Nakuru, ni wa tatu kwa pointi 23 huku Tusker wakisalia nafasi ya tano kwa alama 22 sawa na Kogalo baada ya kulambishwa bao moja na Kakamega Homeboyz ugani kwao Ruaraka kwenye mtanange mwingine uliogaragazwa alasiri ya leo.

Kocha na tena mchezaji wa Homeboyz Allan Wanga alicheka na nyavu bao la kipekee dakika nne kabla ya kipindi cha mapumziko.

Katika kaunti ya Bungoma, wageni Chemelil Sugar waliinyuka Nzoia Sugar 1-0 shukrani kwa goli lake Justine Monda.

Hapo kesho, AFC Leopards wanawakaribisha Ulinzi Stars ugani Machakos kwenye ngarambe iliyosubiriwa na wengi. Leopards watahitajika Kuonyesha kama kweli wamepata motisha ya kuahidiwa posho lao na wizara ya michezo kupitia waziri Rashid Echesa aliyekutana na viongozi wao juzi.

Ingwe wamepoteza mechi nne zilizopita, matokeo yaliyowaacha nafasi ya pili kutoka mkiani mwa jedwali.

Author: Vincent Stephen