Sheria Kutungwa Kuzuia Upangaji wa Matokeo Kwenye Michezo Kenya

157

Bunge la Jamhuri ya Taifa la Kenya kupitia kwa Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Michezo na Utamaduni nchini humo limeahidi kuanza mchakato wa kutunga sheria itakayokuwa inazuia vikali vitendo vya mtu au taasisi kujihusisha na upangaji wa matokeo michezoni.

Mpango wa serikali unafuatia kikao Leo kati ya Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini Kenya Nick Mwendwa, Mtendaji Mkuu wa FKF Barry Otieno na Katibu wa Michezo Jonathan Mueke ambapo baada ya kikao hicho Katibu huyo amesema wataanza mchakato wa kushawishi kabla ya bunge kupitisha.

Taifa la Kenya limekuwa likikumbwa na matukio ya upangaji wa matokeo ambapo mpaka sasa Shirikisho la Kandanda limewafungia wachezaji 8 na waamuzi 25 kutokana na vitendo vya kibaguzi, hata hivyo hukosa makali kutokana na sheria kukosa meno.

“Kunapokuwa na upangaji wa matokeo, mashabiki hupotea viwanjani jambo ambalo ni hatari sana kwa afya ya soka”, alisema Mwendwa wakati akiongea kwenye kikao hicho.

“Shirikisho linachukua hatua kwa uwezo wetu lakini kuna wahusika ambao wako nje ya uwezo wetu, tunahitaji sheria ambayo itamgusa kila mmoja”, aliongeza.

Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Michezo na Utamaduni Jonathan Mueke akielezea maombi ya Rais wa FKFPL amesema kila kitu kitafanyika kwa haraka kulingana na mahitaji makubwa yaliyopo.

“Tutafanya sasa, tutafanya mswada kisha hatua nyingine zitaendelea kama kawaida”, alisema.

Author: Asifiwe Mbembela