Shomari Kapombe kukosa mtanange dhidi ya Lesotho

Mlinzi wa kulia wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Shomari Kapombe ataukosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Lesotho Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon dhidi ya wenyeji Lesotho kutokana na kuwa majeruhi.

Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Jumapili November 18, 2018 Uwanja wa Setsoto mjini Maseru kuanzia Saa 11:00 jioni na Kapombe anayeweza kucheza kama kiungo pia hataweza kucheza kutokana na maumivu ya enka. Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Maseru kwamba Kapombe aliumia juzi katika mazoezi ya jioni kwenye kambi ya Bloemfontein, Afrika Kusini.

Msangi amesema kwamba Kapombe aliukanyaga mpira vibaya, mguu ukacheza na kusababisha maumivu ya kifundo cha mguu na pamoja na jitihada za madakatri wa timu, Richard Yomba na Gilbert Kigadya kumtibu, lakini hajapata nafuu na imethibitishwa hatacheza keshokutwa.

Shomari Kapombe anaungana na Mbwana Ally Samatta ambaye pia ataukosa mchezo huo kutokana na kuonyeshwa kadi mbili katika mchezo dhidi ya Uganda na Cape Verde.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments