Sikazwe Kuchezesha Fainali ya Shirikisho Afrika, Orlando Pirates V RS Berkane

606

Shirikisho la Soka barani Afrika Caf limemteua Janny Sikazwe kuwa ndiye refarii mkuu wa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho baina ya Orlando Pirates na RS Berkane, mtanange utakaopigwa Ijumaa hii, uwanja wa Godswill Akpabio uliopo mji wa Uyo, Nigeria.

Kutajwa kwa Sikazwe ambaye ni mwamuzi mwenye beji ya Fifa kumeibua maswali kwa wadau wa mpira kufuatia refarii huyo kufanya makosa ya kumaliza mchezo wa Afcon 2021 Cameroon baina ya Tunisia na Mali dakika ya 85 kisha kuazisha tena mchezo kabla ya kumaliza kabla ya muda uliongezwa.

Refarii huyo raia wa Zambia atasaidiwa na refarii wa Angola Jerson Emiliano Dos Santos na Arsenio Chadreque Maringule ambaye ni raia wa Msumbiji wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Joshua Bondo kutokea Botswana.

Sikazwe ni moja ya marefarii wenye hadhi kubwa barani Afrika ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kuchezesha mashindano makubwa kama Kombe la Dunia mara kadhaa mathalani mwaka 2016, 2018 na fainali za mwaka huu 2022 pia ameteuliwa kuwa sehemu ya waamuzi kutokea barani Afrika kwenda huko Qatar.

Orlando watahitaji kushinda taji la Shirikisho baada ya mwaka 2015 kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Étoile du Sahel ya Tunisia wakati RS Berkane watahitaji taji tena baada ya kushinda kwa mara ya kwanza mwaka 2020.

Author: Asifiwe Mbembela