Simba haikamatiki, yaifyatua Ruvu Shooting 3-0

Mwendo ni ule ule kwa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu ya Simba baada ya kuendelea kuvuna alama kwenye kila mchezo uliombele yake, ikivunja uteja kwa Ruvu Shooting yaitwanga 3-0 mchezo uliopigwa dimba la CCM Kirumba Jijini Mwanza Juni 3.
Licha ya kuwa mchezo wenye ushindani lakini ulipambwa zaidi katika midomo ya wasemaji, Ruvu Shooting ikitamba kupitia kwa Masau Bwire wakati Simba ikitumia mashabiki pamoja na Haji Sunday Manara.
Mshambuliaji na nahodha wa Simba John Bocco amekuwa kwenye ubora mkubwa tangia kuanza kurejea kwenye kikosi baada ya majeruhi, aliingia kambani mara mbili kunako dakika ya 17 na 87.
Bao la tatu ni mali ya Chris Mugalu dakika ya 61 ambaye aliwafanya mashabiki wa Simba kuongeza shangwe na kusepa na pointi tatu baada ya kumaliza shambulio la haraka la Luis Jose Miquissone na Bernard Morrison.
Ushindi huo ni kama Simba imevunja uteja na Ruvu Shooting hasa ikichagizwa kuwa mtanange wa raundi ya kwanza uliopigwa dimba la Uhuru Dar es Salaam, Simba iliangukia pua kwa kuchapwa 1-0.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares