Simba hoi mbele ya Kagera Sugar

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu Tanzania bara Simba Ijumaa wameangukia pua dhidi ya Kagera Sugar katika mtanange uliochezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa goli 1-0, Kagera ikiendelea na rekodi bora kwa Simba.

Mpaka dakika 90 zinamalizika za mwamuzi ambapo Simba wako nyuma kwa goli moja kwa bila hawakuamini kilichotokea huku wakitupiana lawama wao wenyewe.

Mtanange huo uliamuliwa na goli la kujifunga la Mohamed Hussein Tshabarara katika dakika ya 42 ya mchezo ikiwa ni baada ya kukosa mawasiliano mazuri baina yake na mlinda mlango Aishi Manula kufuatia mpira uliopigwa na mchezaji wa Kagera.

Mbali na Simba kutawala sehemu kubwa ya mchezo kwa maana ya umiliki wa mpira, kona, michumo, Kagera Sugar walionekana kulinda kwa umakini zaidi lango haswa baada ya kupata bao la kuongoza na kuwafanya Simba kushindwa kucheka na nyavu zao.

Kocha wa Simba Patrick Aussems aliwafanyia mabadiliko wachezaji Hassan Dilunga nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Juma huku James Kotei naye akitolewa na Jonas Mkude akichukua nafasi yake, ikiwa ndio mwanzo wa kipindi cha pili kinaanza.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kusalia nafasi ya kwanza wakiwa na alama zao 81 kwenye nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi huku Kagera wakijiongezea alama tatu muhimu wakifikisha alama 43.

Kagera Sugar imefanikiwa kuvuna alama 9 katika michezo 4 ambayo timu hizo zimekutana, huku msimu wa 2018/19 Simba haijafanikiwa kuvuna hata alama moja mbele ya Kagera Sugar.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends