Simba, Kagera zamalizana na Mhilu

Baada ya usajili wake kuzua sintofahamu kubwa kutokana na klabu mama kudai kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu ya Simba haijafuata utaratibu, hatimaye winga Yusuph Mhilu ni mali ya Simba kufuatia Kagera Sugar (klabu mama) kukiri kumalizana na klabu hiyo.

Usajili huo umekamilika baada ya Simba kuweka kitita kirefu cha fedha mezani na kulainisha mazungumzo baina ya pande mbili ambazo zilikuwa zinahitarafiana tangia mchezaji huyo kuonekana kutambulishwa muda mfupi baada ya kambi ya timu ya taifa yenye chini ya miaka 23 kuvunjwa.

Taarifa rasmi kutoka Kagera Sugar imeeleza kuwa: “Tumefikia makubaliano ya pande zote mbili (Kagera Sugar FC na Simba SC) juu ya uhamisho wa aliyekuwa mchezaji wetu Nyota Yusuph Valentine Mhilu kwa Dau la Tsh.40M.

“Yusuph Mhilu alisaini kandarasi ya miaka miwili kuitumikia Kagera Sugar Football Club mwaka jana 2020. Hivyo uhamisho huu wa Yusuph Mhilu kwenda Simba ni Uhamisho ambao umehusisha kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja uliosalia ndani ya Klabu ya Kagera Sugar.

“Tunamtakia kila la kheri huko aendako na Mungu amsimamie katika kukiendeleza kipaji chake,”

Alisaini dili la miaka mitatu jambo ambalo liliwafanya mabosi wa Kagera Sugar kushangazwa na suala hilo la utambulisho kwa kuwa hakukuwa na taarifa kwao.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares