Simba Kurejea Uwanjani Leo Jumapili

477

Baada ya mapumziko ya siku tano, Leo Jumapili wachezaji wa Simba wanarejea kambini kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la TFF na Kombe la Shirikisho Afrika ambayo itaendelea baada ya kalenda ya Fifa kumalizika.

Uongozi wa Simba kupitia kwa kocha Pablo Franco Martin ulitoa ruhusa ya mapumziko kwa wachezaji ambao hawakwenda kwenye majukumu ya timu za taifa na kutakiwa kurejea Leo kambini na kuanza mazoezi kujifua.

Mchezo wa kwanza kwa Simba baada ya kalenda ya Fifa utakuwa dhidi ya US Gendarmerie mchezo utakaochezwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa mwisho kwa Simba Kundi D ambao wanahitaji alama tatu kufuzu robo fainali.

Mapema kabla ya mapumziko, Kocha Pablo aliwaeleza wasiokuwa katika majukumu ya timu ya taifa wanatakiwa kulinda utimamu wa miili kama walivyoachana mara ya mwisho maana mziki wanaokwenda kuuanza sio masihara.

Simba watacheza mechi ya mwisho hatua ya makundi dhidi ya USGN, Aprili 3 Uwanja wa Benjamin Mkapa na wanahitaji ushindi ili kuwa na uhakika wa kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Author: Asifiwe Mbembela