Simba kutua Botswana bila Mugalu, Mhilu

Wakati ikifahamika kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu ya Simba wataondoka kesho Ijumaa Octoba 15 kuelekea Botswana kumenyana vikali na Jwaneng Galaxy Fc, imefahamika kuwa klabu hiyo itakosa huduma ya mshambuliaji wa kati Chris Mugalu na winga wa zamani wa Kagera Sugar Yusuph Mhilu.

Simba inaondoka kwenda kuanza rasmi kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kwa mjibu wa kocha Didier Gomes Da Rosa amesema wanampango ya kufika hatua ya nusu fainali.

Kocha Didier Gomes amesema Mugalu hatakuwa sehemu ya mchezo wa Jumapili, kwani hajafanya mazoezi na wenzake.

“Ana majeruhi na hayupo mazoezi hivyo hataweza kusafiri na timu. Aliumia mazoezini wakati tukijiandaa na mechi na Biashara na hakucheza mchezo huo lakini tukamchezesha mechi iliyofuata ya Dodoma Jiji na akajitonesha,” alisema Gomes.

“Pia katika mchezo huo tutamkosa Yusuf Mhilu ambaye alichelewa kwenye usajili wa kimataifa,” amesema Gomes.

Gomes amesema hana shaka juu ya kikosi chake kwani kimejiandaa vizuri kushinda mchezo huo ili kutimiza malengo yao ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo na kufika mbali zaidi.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends