Simba Mabingwa Kombe la Mapinduzi 2022

386

Simba imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi. Goli la penalti la mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere limeipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi Leo Alhamis Januari 13 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kagere alifunga bao hilo dakika ya 56 baada ya winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho kugongana na kipa Mganda wa Azam, Mathias Kigonya na hilo linakuwa taji la nne la Mapinduzi kwa Simba baada ya awali kulibeba mwaka 2008, 2011 na 2015.

Baada ya mchezo, beki Mkongo, Hennock Inonga Baka ‘Varane’ alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi, wakati winga Sakho alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mashindano na chipukizi Tepsi Evance wa Azam FC alipewa Tuzo ya Mchezo wa Kiungwana.

Baka na Sakho kila mmoja amepewa Sh. Milioni 2, wakati Tepsi alipewa Sh. 300,000.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi alimkabidhi Nahodha wa Simba Kombe na mfano wa Hundi ya Sh. Milioni 25, wakati Azam FC walipewa Sh. Milioni 15.

Author: Asifiwe Mbembela