Simba na Yanga zatambiana kuelekea Kariakoo Derby

Joto la pambano la jadi kati ya Simba na Yanga mtanange wa Ligi kuu Tanzania bara limeendelea kutanda miongoni mwa mashabiki wa timu hizo mbili huku yakiwa yamesalia masaa kadhaa kufikia muda wa mchezo huo.

Kabumbu lenyewe ni kesho Jumamosi Januari 4 majira ya saa 11 jioni katika dimba la Mkapa ambapo Simba ndiyo itakuwa  mwenyeji wa mchezo huo wa awali katika raundi ya kwanza.

Joto la pambano hilo linapanda hasa kwa mashabiki lakini Makocha na Manahodha wa timu hizi mbili kwa kila mmoja amejigamba kutoka na ushindi kwenye mchuano huo.

Nahodha wa Simba John Raphael Bocco licha ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeruhi lakini amewataka mashabiki kujitokeza ili kuhanikiza ushindi wa Wekundu wa Msimbazi hao.

“Tunaamini mashabiki ni wachezaji wa 12 hivyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi. Tunaenda kupambana sababu ya timu, tunaenda kutafuta alama tatu ili tuendelee kusalia kileleni. Tunaamini kwa juhudi zetu kama Simba na Mungu akitusaidia tutaibuka na ushindi.” John alisema mbele ya Wanahabari.

Aidha, Juma Abdul amesema timu imejipanga vyema kutoka na ushindi hivyo mashabiki wajitokeza kwa wingi ili kutoa morali ya ushindi kwa timu yao.

“Mashabiki wajitokeza kwa wingi maana sisi(wao) kama wachezaji tumejiandaa vyema kufanya vizuri wala msitishwe na maneno ya mtandao wanayoyasema watu wa Simba” amesema Abdul ambaye licha ya kuwa nadhodha wa Yanga amekuwa hana nafasi ya kudumu kunako kikosi hicho.

Simba na Yanga zimekuwa katika utani wa siku nyingi huku historia ikionyesha ukaribu wa timu hizi sambamba na kufanana kwa sababu za uanzishwaji wake ndiyo unaopelekea utani huo kuendelea kudumu kwa miaka mingi.

Matokeo ya mchezo huo yatakuwa na maana kwa timu zote mbili katika wakati huu kwani Yanga ina matamanio ya kushika nafasi ya pili na baadae ya kwanza huku Simba ikihitaji kuendeleza utawala wa kuongoza msimamo wa TPL

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares