Simba waogelea fedha ndefu kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika

Wekundu wa Msimbazi Simba wamepata fedha nzito baada ya kuwaondosha AS Vita Club ya Congo na kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mchezo uliopigwa dimba la Mkapa Leo Jumamosi kumalizika kwa faida yao ya goli 4-1.

Awali kabla ya mchezo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, ambaye pia ni mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, alitoa ahadi kuwa endapo watashinda watapata kiasi cha shilingi milioni 600 kama zawadi na motisha kuelekea mechi za robo fainali ya mashindano hayo.

Katika mchezo wa Leo Simba imepata goli zake kupitia kwa Luis Miquissone, Clatous Chama aliyefunga goli mbili na Larry Bwalya aliyepigilia msumali wa mwisho.

Simba wanafikisha alama 13 katika mechi tano ambazo wamecheza, Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi hiyo wanaalama 8, Vita Club alama 4 na Al-Merrikh pointi 2.

Kabla ya mchezo huo, michezo yote ya makundi ambayo Simba ilikuwa inacheza ilikuwa inatengewa kitita cha milioni 200 ambazo hutumika kama motisha kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uwekezaji.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares