Simba wapigwa STOP kuwapeleka mashabiki kwa Mkapa dhidi ya Al-Merrikh

Kuelekea mtanange wa siku ya Jumanne Machi 16 wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu ya Simba imesema kuwa itacheza bila mashabiki katika mchezo huo dhidi ya Al-Merrikh utakaopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dsm.

Licha ya kwamba kulikuwa na katazo la mashabiki kwa timu nyingi ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ila kwa Simba walikuwa wanapata kibali cha kuingiza nusu ya mashabiki, tayari waliingiza katika mechi ya Al Ahly.

Hii ilikuwa ni kwa sababu ya kuchukua tahadhari ya Virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia.

Leo Machi 13, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema wakati wakiwa kwenye maandalizi ya mechi hiyo itakayokuwa na ushindani mkubwa wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kwamba hawataruhusiwa kuwa na mashabiki.

“Tukiwa kwenye maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Al-Merrikh hapo tulipokea taarifa kutoka TFF kwamba hatutaruhusiwa kuwa na mashabiki, hivyo hii ni taarifa mashabiki wetu watuwie radhi”, amesema.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Machi 6, Simba ililazimisha sare ya bila kufungana ikiwa ugenini, na sasa ina kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo wa pili ili kuweza kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya nane bora.

Kibindoni kwenye kundi A ina pointi 7 inakutana na Al-Merrikh yenye alama moja.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares