Simba wasema ubingwa ni matokeo ya Uwekezaji

Simba imekabidhiwa taji la Ligi Kuu Bara baada ya kukamilisha mzunguko wa pili kwa msimu wa 2020/21 kwa ushindi mnono wa goli 4-0 dhidi ya Namungo Fc mtanange uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 83 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile.
Namungo inabaki na pointi zake 43 na msimu huu wa 2020/21 imekwama kupata pointi hata moja mbele ya Simba katika mechi zote mbili raundi ya kwanza na ya pili, itakumbukwa mchezo wa awali Simba ilishinda bao 3-1.
Mabingwa hao wa ligi wamefanikiwa kutwaa taji hilo mara nne mfulilizo ambapo Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa sababu ya kufanya hivyo ni uwekezaji mzuri.
“Uwekezaji mzuri kwa wachezaji pamoja na sapoti ambayo tunapata kutoka kwa mashabiki ni nguvu kwetu kuona kwamba tunashinda mechi ambazo tunacheza.
“Hakuna namna shukrani kwa mashabiki kwa jambo hili na tunaamini kwamba msimu ujao utakuwa wa tofauti zaidi,” .
Simba kwa sasa itaendelea kuwa kambini kujiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Azam dhidi ya Yanga utakaopigwa Julai 25 mkoani Kigoma kufikia rekodi ya msimu uliopita wa kushinda taji la ASFC kwa kuifunga Namungo pia.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares