Simba yainyamazisha Ruvu Shooting Mwanza

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kandanda Tanzania Bara Simba imevuna alama tatu muhimu mbele ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi uliopigwa dimba la CCM Kirumba Mwanza Ijumaa Novemba 19, 2021 kwa ushindi wa goli 3-1.

Simba ambayo iliuanza mchezo huo kwa kasi ya juu na kukaba kwa nguvu ilipata mabao yake matatu ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza yakifungwa na Meddie Kagere mawili na Kibu Denis huku Ruvu wakifunga bao pekee kupitia kwa Elias Maguli.

Mabao hayo mawili yanamfanya Kagere kufikisha manne akiongoza orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu akiwa na idadi sawa na Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania.

Ruvu Shooting walipata bao la kufutia machozi mnamo dakika ya 70 likifungwa na Elias Maguli aliyetumia vyema makosa ya walinzi wa Simba waliofanya makosa kuondoa mpira uliokuwa unazagaa langoni mwao.

Bao hilo linaharibu rekodi ya Manula ya kucheza mechi tano bila kuruhusu bao, ambapo kabla ya hapo alikuwa amecheza mechi tano sawa na dakika 450 bila kuruhusu bao.

Hata hivyo Simba walikosa mkwaju wa penalti katika dakika ya 72 ukipigwa na Erasto Nyoni lakini kipa wa Ruvu Shooting Mohamed Makaka aliuokoa.

Ushindi huo wa mabao matatu unaendeleza rekodi ya Simba mbele ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana Juni 3 mwaka huu Simba wakishinda kwa mabao 3-0.

Simba wanafikisha pointi 14 wakikamata nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wenye alama 15, ambao watakuwa na mchezo kesho Jumamosi Novemba 20, dhidi ya Namungo Fc ya Lindi.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends