Simba yaiva kuwavaa Red Arrows ya Zambia

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu ya Simba imesema inaendelea vyema na maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia mchezo utakaopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Jumapili Novemba 28, 2021.

Simba ambayo itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa kwanza, atatakiwa kujipa angalau uhakika wa ushindi kwenye mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kwenda Zambia katika mechi ya mkondo wa pili.

Kuelekea mchezo huo, Mwenyekiti wa Simba Murtanza Mangungu amesema upande wa uongozi wamekamilisha utaratibu wa maandalizi kuelekea mchezo husika, huku wakiamini ushindi utapatikana siku ya Jumapili.

Amesema uongozi umefanya kila kitu kinachohitajika upande wa timu na maandalizi mengine ambayo ni maagizo kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’.

“Kwa sasa Kocha anaendelea kuwapa mbinu wachezaji na nina amini kwamba kwa umuhimu wa mashindano ya kimataifa tutafanya vizuri na kupata matokeo.”

Simba iliangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi Mabingwa Barani Afrika na Jwaneng Galaxy Fc kwa faida ya goli la ugenini baada ya sare ya goli 3-3, Simba ilishinda 2-0 Botswana raundi ya kwanza kabla ya kukubali kufungwa 3-1 DSM.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends