Simba yakabidhiwa ubingwa wa VPL Lindi licha ya sare dhidi ya Namungo

491

Simba SC imekabidhiwa rasmi leo Julai nane 2020 taji lao la VPL baada ya kutwaa taji hilo wiki iliyopita kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Taji hilo wamekabidhiwa katika dimba la Majaliwa mkoani Lindi waliokuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Namungo FC mtanange ambao umeisha kwa sare tasa na kufikisha alama 81.

Uongozi wa Simba umesema kuwa shukran kubwa za kutwaa ubingwa wanazirejesha kwa Mungu pamoja na mashabiki wa Klabu hiyo kwa kuipa sapoti mwanzo mwisho.

Ofisa Habari wa Simba,  Haji Manara amesema kuwa anaamini ni mpango wa Mungu kutwaa ubingwa pamoja na sapoti kubwa ya mashabiki.

“Wamekuwa nasi bega kwa bega mashabiki kwenye kazi kubwa ambayo wachezaji walikuwa wakifanya kwa namna yoyote ile wanahitaji pongezi na wanastahili  haya tunayoyapata kwa sasa,” amesema.

Huu ni ubingwa wa 21 kwa Simba inayonolewa na Sven Vandenbroeck,  na Kocha Msaidizi Seleman Matola.

Author: Asifiwe Mbembela