Simba yalamba sukari ya Kagera, Kagere akitoa salamu Kombe la TFF

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho la TFF wamefanikiwa kutinga  robo fainali ya Kombe hilo baada ya kuitandika Kagera Sugar bao 2-1 mtanange uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Leo Jumamosi.

Kagera Sugar walikuwa wa kwanza kufunga goli kupitia kwa winga machachari Eric Mwaijage akimalizia krosi maridhawa ya beki nambari mbili za Kagera Sugar kunako dakika ya 45 ya mchezo.

Hata hivyo, Simba waliingia uwanjani kipindi cha pili wakiwa na nguvu zaidi na kufanikiwa kusawazisha bao na kuongeza lingine linalowafanya wapite na kutinga hatua ya robo fainali.

Ni Bernard Morrison ambaye alipachika bao la kuweka usawa dakika ya 56 na lile la ushindi lilipachikwa na Meddie Kagere ambaye alitumia pasi mpenyezo ya Morrison.

Kipindi cha pili Simba, Didier Gomes ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo aliamua kubadili mbinu kwa kuwatumia washambuliaji wawili ambao ni Meddie Kagere na John Bocco ili kuongeza mashambulizi.

Kwa upande wa viungo aliamua kumuingiza Bernard ambaye aliweza kutimiza majukumu kwa wakati na kuwafanya Kagera Sugar washindwe kuhimili kasi ya wachezaji hao wanaowania taji hilo ambalo lipo mikononi mwao.

Kutinga kwao hatua ya robo fainali kunawafanya waungane na watani zao wa jadi Yanga ambao Jana, Aprili 30 walitangulia baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Nelson Mandela.

Ushindi huo unaweza kuwa salamu kwa watani wa jadi Yanga kwani hapa katikati hakutakuwa na mechi yoyote zaidi ya hiyo ya Jmamosi Mei 8.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares