Simba, Yanga Zatambiana Kariakoo Derby

319

Manahodha wa klabu ya Simba na Yanga wameonyesha kujiamini dhidi ya mwenzake kufuatia kutoa kauli nzito kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mtanange utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, April 16.

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ nahodha msaidizi wa Wanalunyasi akizungumzia mchezo wa kesho ameeleza kuwa bado wapo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hivyo mchezo dhidi ya watani wa jadi, Yanga ni muhimu kushinda kesho ili kujiweka sawa.

Tshabalala ameongeza kuwa wanajua endapo watapoteza watakuwa wamepoteza ubingwa wa Ligi tena msimu huu.

Kiungo mkabaji wa Yanga Mudathir Yahya Abbas amesema wao kama wachezaji wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.

Mbali na wachezaji, makocha nao pia wameeleza maandalizi yao ya mchezo wa kesho ambao utakufanyika saa 11 jioni.

Mbrazil wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amesema Simba haiwezi kubadili chochote kwenye mchezo huo, bali wataingia na mkakati maalum wa ushindi.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze amesema mechi ya kesho ni ya wapinzani na kila upande una motisha yake, hivyo kwa upande wao wamejiandaa kwa utulivu na wako vizuri kuelekea mchezo huo.

Wakati homa ya mchezo huo ikipanda, Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 68, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 60 baada ya wote kucheza mechi 25.

Author: Asifiwe Mbembela