Simba yaondolewa ligi ya mabingwa na UD Songo

“Mipango sio matumizi” Waswahili ndivyo mara nyingi wamekuwa wakiutumia usemi huo kuonyesha kutofanikiwa kwa mambo mbalimbali katika maisha.

Ndio! mipango sio matumizi. Baada ya Simba kukusudia kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu 2019/20 baada ya msimu 2018/2019 kufika robo fainali lakini sasa mambo yameenda kombo.

Mabingwa watetezi wa TPL Simba wametolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye mchezo wa marudio uliochezwa uwanja wa Taifa dhidi ya UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya goli 1-1, Songo wakitumia faida ya goli la ugenini.

Songo walikuwa wa kwanza kuandika goli kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na nahodha Luis kunako dakika ya 14 baada ya uzembe wa mabeki na mlinda mlango Aishi Manula ambao waliusindikiza kwa macho mpira nyavuni.

Bao lao la usiku la penati lililofungwa na Erasto Nyoni dakika ya 87 halikusaidia kuivusha hatua inayofuata kwa kukosa faida ya goli kwenye mchezo wa awali.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kuungana na KMC kuaga mashindano ya kimataifa kwani nao waliotolewa uwanja wa Taifa kwa kufungwa mabao 2-1 na AS Kigali.

Kwa Tanzania bara hivi sasa itawakilishwa na Yanga ligi ya mabingwa na Azam kombe la shirikisho.

Patrick Aussems, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa haikuwa bahati yao leo kushinda kwani wamepoteza nafasi nyingi za wazi.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends