Simba yapaa kuwakabili Al Ahly Ligi ya Mabingwa Afrika

Kikosi cha Simba kimeondoka nchini Tanzania Aprili 6, 2021 kuelekea Misri kucheza mechi ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mabingwa watetezi wa CAFCL Al Ahly mchezo unaotarajiwa kupigwa Aprili 9.

Akizungumzia safari hiyo Meneja wa timu ya Simba Patrick Rweyemamu amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Al Ahly unaotarajiwa kuchezwa Aprili 9, nchini Misri.

“Tunashukuru Mungu tumekuwa tukipata matokeo mazuri kwenye mechi za kimataifa, kikubwa ambacho tunaamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika mechi yetu ya mwisho.

“Wachezaji ambao tupo nao wapo tayari na wanahitaji kufanya vizuri tunaamini itakuwa hivyo, Watanzania na wadau watuombee ili tukafanya vizuri, ” amesema.

Simba imeshafuzu kucheza robo fainali ya Ligi hiyo baada ya kufikisha alama 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu iliyo nafasi ya pili, tatu wala nne, inaenda Misri kukamilisha ratiba.

Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye msafara wa leo ni pamoja na Luis Miquissone, Clatous Chama, Ibrahim Ajibu, Ally Salim, John Bocco na Beno Kakolanya.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends