Simba yashinda tena Afrika Kusini

49
Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa goli 4-1 dhidi ya Platinum Starz ya Afrika Kusini ukiwa ni mwendelezo wa michezo ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya wa mashindano 2019/20 unaotegemewa kuanza baadae mwezi Agosti.
Unakuwa ni mtanange wa pili mfululizo kwa Simba Sports Club kucheza baada ya hapo jana(Jumanne, Julai 23) klabu hiyo kushinda mabao 4-0 dhidi ya Orbert TVET. Katika mchezo wa leo magoli ya Wanamsimbazi hao yamefungwa na Mzambia Clatous Chota Chama ambaye amefunga goli 2 dakika ya 11 na 58 katika ushindi wa goli nne. Goli nyingine mbili zimefungwa na Kiungo mkabaji wa Sudani Sharif Shaboub kunako dakika ya 13 kwa njia ya penati na goli la mwisho limefungwa na Kiungo mchezeshaji Mzamiru Yasni dakika ya 87 ya mchezo huo.
Goli pekee ya Platinum Stars limefungwa na Ruele dakika ya 75 ya mchezo. Baada ya mchezo huo Simba inakabiliwa na michezo miwili ya mwisho ambayo ni migumu zaidi kutokana na historia ya hizo timu Julai 27 dhidi ya Townships Rollers na 30 Julai dhidi ya Orlando Pirates.

Author: Bruce Amani