Simba yatinga hatua ya makundi ya Kombe la Klabu bingwa Afrika

704

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya kandanda nchini Tanzania Simba SC wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kuifurusha Nkana FC kwa jumla ya goli 4-3 katika michezo ya raundi zote mbili, mtanange uliofanyika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa leo Simba ilihitaji kushinda hata kwa goli moja baada ya mchezo wa awali uliofanyika Kitwe Zambia kupoteza kwa goli mbili kwa moja.

Simba iliwalazimu kukubali kutanguliwa goli moja lililofungwa na nahodha wa Nkana FC Walter Bwalya kunako dakika ya 16 baada ya walinzi kuzubaa kwa kushindwa kuondosha majalo mjarabu kutoka kwa Musa Mayeko Mohamed na hivyo kuwa na mlima mrefu zaidi wa kupanda ambapo mwisho mwa dakika za mwamuzi Peter Waweru kutoka Kenya ziliwaonyesha Simba kuwa kileleni kwa kufanikiwa kurudisha goli na kuongeza mengine.

Magoli ya Simba yalifungwa na Jonus Gerrard Mkude, Meddie Kagere, na wakati goli la Clatous Chota Chama likifungwa dakika za lala salama akipokea mgongea kutoka kwa HD Hassan Dilunga.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 2013/04 na kuendelea kudhihirisha ubora wao pamoja na uwekezaji wa billion 1.3 kutoka kwa muwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo’

Aidha, Nkana FC inaangukia kwenye Kombe la shirikisho ambako italazimika kucheza mchezo wa mtoano kabla ya kuingia kwenye makundi yenyewe na endapo haitashinda itakuwa imeondoshwa moja kwa moja.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko kadhaa ambapo Nkana alitoka Kelvin Kampamba na kuingia Chisamba Lungu, alitoka Ronald Kampamba na kuingia Freddy Tshimenga.

Simba alitoka Kagere akaingia Dilunga, Okwi akaingia Kichuya na aliingia Jurko Murshid akatoka Nicholaus Gyan

Author: Bruce Amani