Simba yatoa somo kwa Dodoma Jiji, yaichapa 3-1

Vinara wa Ligi Kuu nchini Tanzania Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika michezo ya VPL baada ya kuitandika Dodoma Jiji FC bao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yamefungwa na mshambuliaji Mkongo, Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 8 akimalizia pasi ya Larry Bwalya kabla ya kusawazishwa bao hilo na kiungo mshambuliaji wa Dodoma Jiji Cleophase Mkandala kunako dakika ya 29.

Hata hivyo, Luis Miquissone aliandikisha bao la pili kwa Simba akimalizia mpira wa kuchopu wa Clatous Chota Chama kabla ya Mugalu kufunga goli la mwisho kwenye mechi hiyo.

Simba SC inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 25 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi nne zaidi ya watani wao jadi, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi.

Dodoma Jiji yenyewe inabaki na pointi zake 38 za mechi 28 sasa katika nafasi ya sita.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares