Simba avamia jangwani na kuponyoka na nyota mwingine

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC wamemtangaza rasmi mlinzi wa Tanzania “Taifa Stars” Gadiel Michael Kamagi Mbaga kuwa mchezaji wao kwa misimu miwili baada ya kuingia kandarasi ya miaka 2 ndani ya klabu hiyo.

Gadiel Michael kabla ajajiunga na Simba alikuwa katika kikosi cha klabu ya Yanga ambapo amedumu kwa miaka miwili akitokea katika timu ya Azam Fc ya jijini Dsm.

Gadiel, 22, amekuwa kwenye mjadala kwenye mitandao ya kijamii kwa takribani wiki mbili sasa huku timu mbili kongwe zikijinadi kupata saini yake. Yanga ikiwa inatajwa kama imekamilisha mazungumzo na mchezaji huyo Simba pia akijinadi kumsainisha, kabla ya leo kutangazwa rasmi kwa Wekundu wa Msimbazi Simba.

Mchezaji huyo anaimdu zaidi nafasi ya beki wa pembeni kushoto, amekuwa katika kiwango kizuri kwenye misimu takribani mitatu toka aje Yanga hata timu ya taifa pia, anaingia Simba kupambania namba na nahodha msaidizi wa Simba Mohammed Hussein Tshabalala ambaye pia anacheza nafasi hiyo.

Gadiel Michael Mbaga anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Simba kutokea Yanga msimu huu baada ya mlinda mlango Beno David Kakolanya ambaye pia alisajiliwa mwezi Juni.

Safari ya Gadiel Michael Kamagi ilianzia kwenye mashindano maalum ya Copa Coca Cola kabla ajajiunga na Azam kwenye timu za watoto (Academy) baadae akajiunga na timu ya wakubwa msimu wa 2014/2015, akaenda Yanga msimu uliofuata kwa mkataba wa miaka miwili na sasa ameingia Simba.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments