Simba yawataka mashabiki kujaza uwanja mchuano dhidi ya Songo

57

Uongozi wa Simba SC umewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya mabingwa Afrika watakapocheza na UD de Songo ya Msumbiji jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili kuanzia saa 10 jioni.

Kuelekea mchezo huo, Simba kupitia kwa Msemaji wa klabu hiyo Haji Sunday Manara imewaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kushuhudia mchezo wa Jumapili ili kuweko na hamasa kama msimu uliopita.

Hali kadhalika, amewataka mashabiki wa Simba kuziunga mkono klabu vya Yanga SC, Kinondoni Municipal Council (KMC) ambayo itacheza Ijumaa na Azam FC Jumamosi. Manara anaamini kufanya vizuri kwa timu hizi kutaendeleza uwakilishi wa nchi nne ngazi ya vilabu.

Wiki ijayo Tanzania itakuwa kwenye pilikapilika ya michezo ambapo klabu zote nne zitakuwa uwanjani kuwania nafasi ya kuendelea kwenye hatua inayofuata kwenye michuano husika, Azam na KMC wataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho na Simba na Yanga wataiwakilisha nchi kwenye Ligi ya mabingwa.

Simba ilitoa suluhu katika mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Msumbiji hivyo wanahitaji ushindi wowote ule ili kusonga mbele kwa hatua inayofuata.

Author: Bruce Amani