Simba yawavaa kibabe miamba Al Ahly, Slogan ya kuwatisha Ahly yawekwa wazi

Klabu ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu nchini Tanzania na Ligi ya Mabingwa Afrika imeendelea kujiandaa na mchezo wa pili wa CAFCL dhidi ya Al Ahly mtanange utakaopigwa Jumanne tarehe 23 katika ardhi ya Tanzania.

Kuelekea mbilinge mbilinge hiyo, Simba kama ilivyo kawaida yake imezindua kauli mbiu ya kuingia kwenye mchezo huo dhidi ya washindi wa tatu wa Kombe la Dunia ngazi ya klabu. Kauli mbiu hiyo inaenda kwa jina la TOTAL WAR: POINT OF NO RETURN. Yaani VITA KAMILI: HAKUNA KURUDI NYUMA

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema wanatambua mchezo utakuwa mgumu ila watapambana kupata matokeo chanya kwa kuwa wamekuwa wakifanya vizuri Uwanja wa Mkapa. “Mabingwa wa Afrika Al Ahly ambao wametoka kushiriki ubingwa wa dunia na kushika nafasi ya tatu watakuja kuwakabili mabingwa mara nyingi zaidi wa Afrika Mashariki ambao ni Simba.

“Rekodi hizo zitaufanya mchezo kuwa wa kipekee ndani ya uwanja na kila mmoja ninatambua kwamba anajua namna ambavyo tunahitaji ushindi.” “Mara ya mwisho tulikutana hapa Dar tukawafunga 1-0 kwenye mechi tuliyosema “YES WE CAN” na tukaweza na mara zote tukicheza Tanzania tunawafunga.

“Al Ahly sio timu nyepesi. Tunaposema tunaweza kuwafunga tunajua ukubwa wao, lakini Simba hupenda mechi kubwa kama hizi. “Mechi ya mwisho tuliita WAR IN DAR, mechi ya jasho na damu ndani ya dakika 90 na sasa tunasema TOTAL WAR: POINT OF NO RETURN hii sasa ni vita kamili ya ndani ya uwanja,”.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends