SPAL yaichelewesha Juve kusherehekea taji la nane la Italia

Juventus walinyimwa Jumamosi nafasi ya kushinda taji la nane mfululizo la Serie A, kufuatia kichapo cha kushangaza cha 2 – 1 dhidi ya SPAL inayopambana kuepuka kushushwa daraja.

Kevin Bonifazi na Sergio Floccari waliifungia SPAL wakati ilitoka nyuma ya kunyakua pointi zote tatu, hivyo kuwafanya Juve kusubiri kwa mara nyingine tena kutawazwa mabingwa wa Italia.

Juve walihitaji tu pointi moja ili kuwa na uhakika wa kushinda ligi na kocha Massimilliano Allegri alifanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake, kwa kuwapumzisha vigogo wake Cristiano Ronaldo, Federico Bernardeschi, Mario Mandzukic, Alex Sandro, Miralem Pjanic, Blaise Matuidi, Leonardo Bonucci na Giorgio Chiellini kabla ya mchuano muhimu wa mkondo wa pili wa robo fainali ya Champions League dhidi ya Ajax.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends